Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

MADAKTARI BINGWA KUTOKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE – MARA WAFIKIA WAGONJWA 500 WILAYA YA SERENGETI.

Posted on: February 10th, 2024

Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Mara wamefanikiwa kuwahudumia wagonjwa 500 katika kambi ya siku tano ya matibabu na uchunguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Serengeti iliyoanza tarehe 05/02/2024 na kukamilika siku ya tarehe 09/02/2024.

Hayo yamesemwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti Dkt. Mohere Mohere Joseph siku ya jana tarehe 09/02/2024 katika hitimisho la kambi ya siku tano ya Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Mara iliyoanza tarehe 05/02/2024 na kuhitimishwa siku ya leo ya tarehe 09/02/2024 katika Hospitali ya Wilaya ya Sengeti.

“Kimsingi tunashukuru sana kwa ujio huu kwani umekuwa na manufaa makubwa sana katika Halmashauri yetu kwasababu wagonjwa wengi sana wamejitokeza kupata huduma na wengi wamekuwa wakisumbuliwa na matatizo ya muda mrefu mpaka sasa tuna takribani ya wagonjwa 500 ambao wamekwisha kupata huduma za kawaida na wagonjwa 40 ambao wameshafanyiwa upasuaji mkubwa na mdogo” Amesema Dkt. Mohere Mohere Joseph Mganga Mfawidhi Hospitali ya Wilaya ya Serengeti.

Aidha, Dkt. Mohere Mohere Joseph amesema kuwa ujio wa Madaktari Bingwa imekuwa ni fursa ya kipekee kwa wananchi wa Wilaya ya Serengeti kwasababu wagonjwa wengi walikuwa wakipata rufaa za kwenda kwenye Hospitali ya Mkoa na Kanda lakini wamekuwa wakishindwa kwenda kwasababu za kiuchumi.

Katika kambi hii iliyowekwa siku tano na Madaktari Bingwa hao walikuwa wakitoa huduma za kibingwa kama kuona wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa mkojo, wagonjwa wote wenye matatizo ya masikio, pua na koo (ENT), Pia wagonjwa wote wenye matatizo yanayohusu upasuaji kama vile uvimbe tumboni, utumbo kujikunja, ngiri, upasuaji wa nyama za kwenye pua pamoja na uvimbe shingoni (goiter), magonjwa ya kinamama na uzazi pamoja na wagonjwa wote wenye matatizo ya mifupa.

Madaktari Bingwa waliyokuepo katika kambi hiyo ni Daktari Bingwa wa upasuaji, Daktari Bingwa wa Mifupa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya kinamama na uzazi.