Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara

HUDUMA ZA MADAKTARI BINGWA ZITAKUWA ENDELEVU ILI KUPUNGUZA GHARAMA ZA MATIBABU KWA WANANCHI

Posted on: February 8th, 2024

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Dkt. Lusubilo David Adam amesema kuwa huduma ya Madaktari Bingwa itakuwa endelevu katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ili kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Ameyasema hayo leo tarehe 09/02/2024 katika hitimisho la kambi ya siku tano ya Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Mara iliyoanza tarehe 05/02/2024 na kuhitimishwa siku ya leo ya tarehe 09/02/2024 katika Hospitali ya Wilaya ya Sengeti.

“Hii program ambayo inasimamiwa na Halmashauri ya wilaya ya Serengeti ikishirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Mara itakuwa ni huduma endelevu lengo kubwa ni kupunguza mzigo kwa wananchi kuweza kupata huduma hizi za kibingwa ambazo kwa maeneo yetu haya zinapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Mara na hospitali ya Kanda ya Bugando-Mwanza” Amesema Dkt. Lusubilo David Adam.

Amesema, wateja wengi waliokuwa wakihitaji huduma hizi wamekuwa wakishindwa kufika katika Hospitali hizo kutokana na kushindwa kuhimili gharama mbalimbali za usafiri ikiwemo na malazi.

Aidha, Dkt. Lusubilo David Adam amesema kuwa serikali imeona kuleta huduma hizi maeneo ya jirani ya wananchi ili waweze kuhudumiwa kwa wakati na kuweza kupunguza gharama za matibabu.

Pia ametoa wito kwa wananchi pale wanapopata taarifa za ujio wa madaktari bingwa waweze kuitikia wito huo ili waweze pata matibabu na wengine kuja kuona afya zao kama ziko sawa.